Nyumba
ya mkazi wa kitongoji cha Lukondo katika kijiji cha Kikundi kata ya
Kiroka, Fikiri Buma ikiwa imebomolewa na kile kilichodaiwa kuwa ni
utekelezaji wa amri ya baraza la nyumba la halmashauri ya Morogoro
Vijijini ambapo zaidi ya nyumba 20 zilibomolewa januari 10 mwaka huu
tarafa ya Mkuyuni mkoani Morogoro.
Mkazi
wa kitongoji cha Lukondo kijiji cha Kikundi kata ya Kiroka Harouna
Chunga (87) akiowaonyesha waandishi wa habari wa kituo cha luninga cha
ITV, Sifuni Mshana mwenye kamera na Michael Msillo bendera ya CCM tawi
la kitongoji hicho namna ilivyochanwa na watu wanaodaiwa kiutekeleza
amri ya kubomoa nyumba katika eneo hilo januari 10 ambapo jumla ya
nyumba 25 zilibomolewa mkoani Morogoro.
Mwenyekiti
wa kitongoji cha Lukondo kijiji cha Kikundi kata ya Kiroka Hamdan
Chawila kulia na mmiliki wa nyumba iliyobomolewa Amina Said (50) kushoto
wakiangalia uhalibifu baada ya nyumba zaidi ya 20 kubomolewa na kile
kilichodaiwa kuwa ni utekelezaji wa amri ya baraza la nyumba la
halmashauri ya Morogoro Vijijini ambapo zaidi ya nyumba 20 zilibomolewa
januari 10 mwaka huu tarafa ya Mkuyuni mkoani Morogoro.
Na Mtanda Blog, Morogoro.
WANANCHI zaidi ya 3,00 wa kitongoji cha Lukonde kijiji cha Kikundi hawana
sehemu ya kuishi baada ya nyumba zao kudaiwa kubomolewa na askari wa
jeshi la polisi ikishirikiana na mgambo kwa madai ya kutekeleza amri ya
baraza la nyumba la halmashauri ya wilaya ya Morogoro ili kupisha ujenzi
wa majosho ya kuogeshea mifugo ya mwekezaji katika tarafa ya Mkuyuni
mkoani hapa.
Katika
tukio hilo lililotokea januari 10 kuanzia majira ya mchana jumla ya
nyumba 25 za wakazi wa kitongoji hicho zinadaiwa kubomolewa kwa madai ya
kupisha ujenzi wa majosho ya kuogeshea mifugo eneo la kitongoji cha
Lukonde chenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3,000.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika eneo la tukio mara baada ya kufanyika kwa
tukio hilo Mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Lukonde, Hamdan Chawila
alisema kuwa jumla ya nyumba 25 zimebomolewa na askari polisi
ikishirikiana na mgambo ili kupisha ujenzi wa josho la kuogeshea mifugo
na kusababisha zaidi ya wananchi 3,00 kukosa sehemu ya kuishi.
Chawila
alisema kuwa tukio hilo hakuna kiongozi wa kitongoji hicho ambaye
ameshirikishwa jambo ambalo wameshangaa kuona askari pamoja na mgambo
wakivamia na kubomoa nyumba hizo huku akieleza kuwa eneo hilo anafahamu
kuwa lina mgogoro na anayedaiwa kuwa ni mwekezaji aliyefahamika kwa jina
la, Profesa Martin Ndabikunze Shem wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine
Morogoro (SUA) huku kesi ya msingi ikiwa imefunguliwa katika mahakama
ya mwanzo Mikese baada ya mgogoro wa muda mrefu.
“Januari
10 mwaka huu majira ya mchana tulivamiwa na askari polisi wakiwa na
mgambo na kubomoa nyumba 25 katika kitongoji changu na kusababisha
wananchi zaidi ya 3,00 kukosa sehemu ya kuisha na kufanyika kwa
uhalibifu wa mali mbalimbali”. Alisema Chawila.
Mmoja
wa wahanga wa tukio hilo, Fikiri Mikidadi Buma alisema kuwa tukio hilo
la kubomolewa nyumba yake pamoja na wenzake limemrudisha nyuma
kimaendeleo ukizingatia tayari alifanikiwa kujenga nyumba iliyoekzwa na
mabati.
Buma
alisema hakuna taarifa zozote juu ya baada ya kubomolewa nyumba zao
katika zoezi la kuwaondoa kwa nguvu lililofanywa na jeshi la polisi,
mgambo pamoja na kundi la vijana wanaodaiwa kushiriki katika tukio hilo.
“Ninachojua
mimi eneo hili lina mgogoro na mwekezaji na kesi ya msingi ipo mahakama
ya mwanzo Mikese lakini nimeshsngazwa kuona askari polisi na mgambo
kuvamia nyumba yangu na kuibomoa zikiwemo na nyumba za wenzangu na
kupata hasara ya mali na wengine kuibiwa fedha katika tukio hilo la
bomoa bomoa”. Alisema Buma.
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alipotakiwa
kuzungumzia tukio hilo alisema kuwa jeshi la polisi halikuhusika katika
ubomoaji wa nyumba hizo na badala yake askari wa jeshi hilo walienda
katika eneo hilo baada ya kutokea kwa vurugu baina ya wananchi na
wanamgambo aliodai walikuwa wanatekeleza amri ya baraza la nyumba la
halmashauri ya wilaya ya Morogoro kubomoa nyumba eneo hilo.
Kwa hisani ya Juma Mtanda Blog