Shamra shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Mlimani City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa
Tanzania, Jakaya Kikwete alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa
uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni waalikwa.
Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo
ndani na nje ya ukumbi huo.
Ulinzi katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita
kiasi ambapo hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi
maalumu, hata angeomba kwa kupiga magoti.
“Hata sisi tumetoka Bagamoyo hadi hapa tuna undugu
kabisa na mkubwa (Rais Kikwete), lakini wametunyima kwa sababu hatuna
kadi,” alilalamika mwanamke mmoja aliyeongozana na wanaume wawili.
Hakuna waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia
ndani ya ukumbi huo, isipokuwa waandishi na wapiga picha maalumu wa
Serikali ambao walipewa vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine walioonekana wakipiga picha ni wanafamilia
ambapo watoto wa kiume wa Rais Kikwete, walionekana wakiwa na kamera
huku wamevalia kanzu nadhifu.
Mfanyakazi mmoja wa Ikulu alipomwona Mwandishi wa
gazeti hili, alimfuata na kumwambia kuwa sherehe hiyo ni ya kibinafsi na
haruhusiwi mwandishi yeyote kufanya kitu chochote.
“Tumenyimwa kuruhusu waandishi kwenye sherehe hii,
sawa wewe ni mwandishi lakini hii ni sherehe binafsi na ya kifamilia,
huruhusiwi kupiga picha yeyote,” alisema mfanyakazi huyo, jina
linahifadhiwa.
Hata hivyo, mwandishi alitumia mbinu kupata picha
za maharusi hao pamoja na matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea
ukumbini hapo.
Wageni wengi waalikwa walianza kuingia ukumbini humo majira ya mchana na wengine waliendelea kuwasili hadi saa 11 za jioni.
Miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliohudhuria
sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais
Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi, Naibu
Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake Jinsia
na Watoto, Sophia Simba