Saturday, January 18, 2014

MIFUKO YA NAILONI YAUA MIFUGO 500 DODOMA

IDADI ya mifugo inayokufa kwa kula mifuko ya nailoni inazidi kuongezeka katika Kata ya Hombolo. Diwani wa Kata ya Hombolo Manispaa ya Dodoma, Mussa Kawea katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi alisema katika kipindi cha wiki mbili mifugo inayokufa imefikia 500 huku wafugaji wengine wakiingia katika umasikini kwa kupoteza ng'ombe zaidi ya 20.
Taarifa za mwanzo zilisema kwamba idadi ya mifugo iliyokufa kwa kula mifuko hiyo ilikuwa 65.
Alisema mifuko hiyo ambayo imezagaa sana eneo la Hombolo kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu zilizochangiwa na uwepo wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo imekuwa chanzo kikubwa cha kuwatia katika umasikini.
Kawea alisema licha ya mvua kuanza kunyesha na majani kuongezeka lakini ng’ombe wamekuwa wakila mifuko hiyo inayozagaa ovyo kutokana na kuwa na ladha ya chumvi chumvi.
Alisema pamoja na wafugaji kulifikisha suala hilo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lakini hakuna kitu chochote kilichofanyika mpaka sasa.
Alisema ni muhimu kwa Serikali ikapiga marufuku utengenezaji wa mifuko hiyo kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa mifugo huku akiwataka wananchi wenye mazoea kuhakikisha kwamba hawaitupi hovyo na wanaichoma.

 
“Hali hii inatishia umasikini kwa wafugaji tunaomba Serikali kuangalia suala hili kwa makini. Alisema, kutokana na vifo vya ng’ombe vinavyotokea kila mara wafugaji wa maeneo hayo wameitaka Serikali kutimiza maagizo wanayoyatoa ikiwemo lile la kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo.
“Serikali ilipiga marufuku utengenezaji wa mifuko ya rambo na kuagiza viwanda vitengeneze mifuko ya karatasi ambayo ni rahisi kuharibiwa baada ya matumizi lakini agizo hilo linaonekana halijazingatiwa,” alisema.
Alipohojiwa hivi karibuni juu ya athari anazopata ng’ombe anapokula mfuko wa plastiki Daktari wa Mifugo mkoani hapa, Goodluck Ndaweka alisema ng’ombe anapokula mfuko wa plastiki husababisha mfuko ule kwenda kufunga utumbo mwembamba jambo ambalo husababisha chakula anachokula kishindwe kupita.
Alisema kutokana na hali hiyo ng’ombe hukonda na hali hiyo hupelekea kifo chake.

Socializer Widget By Blogger Yard
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →