Nilipofikiria
kuandika makala kuhusu uwezo wa kushawishi watu wengine wakubaliane na
mawazo yetu niliingiwa na shaka kuwa huenda baadhi ya watu wasione
umuhimu wa mtu kuwa na stadi kama hizo. Iwapo wewe ni miongoni mwa watu
wenye fikra hizi, jiulize kama unaweza kuishi bila kuongea na watu, Je,
huwa haitokei ukamweleza mtu au watu mawazo ambayo ungependelea
wayaelewe na kuafikiana na wewe.
Katika
maisha yetu ya kila siku tunatoa maelezo mbalimbali ili kueleza maoni,
fikra ama hisia zetu. Mara nyingine wale tunaoongea nao huwa na mawazo
tofauti na yetu. Hakika hufurahi sana tunapofanikiwa kuwashawishi hadi
wakaafikiana na mawazo yetu. Kuna matukio ambayo hutufanya tuone ni
muhimu sana kuweza kushawisha watu wakubaliane na mawazo yetu. Matukio
hayo ni kama tunapokwenda kwenye ofisi mbalimbali tukiwa na mahitaji
kama vile kiwanja cha kujenga nyumba, nafasi za watoto shuleni,
kuunganisha huduma ya maji au umeme katika nyumba, kuomba mkopo au kazi
na maombi mengine .
Ushawishi
huweza kuwa muhimu zaidi tunapowaeleza watoto wafuate maadili,
tunapomweleza bosi uzito wa kazi na nakuomba nyongeza ya mshahara,
tunapotoa maelezo katika mashauri mahakama au tunapowapatanisha ndugu au
jamaa waliohitilafiana na kukosana. Kuna watu wasiyo na uwezo kabisa wa
kushawishi. Hivyo, badala ya kunasihi, wao hutumia mbinu ya kukaripia
au kufoka. Ushawishi wa namna hii huwa siyo wa hiari wala kudumu. Watu
wenye uwezo mkubwa wa kushawishi huwa na haiba kubwa katika maisha.
Lakini kila mmoja wetu unaweza kujifunza jinsi ya kushawishi.
Wanafalsafa wamefanya utafiti na kugundua kuwa uwezo wa kushawishi
huweza kujengeka kwa kuzingatia mbinu sita zifuatazo:-
Kutumia ushawishi katika sehemu uliyozoea
Watu
wenye uhodari wa kushawishi huweza kufanya shughuli hiyo katika
mazingira waliyoyazoea. Kanuni hii hutumika katika utawala. Mameneja
hufanya vikao na watendaji wao katika ofisi zao. Kama unaongea na mtu au
kundi ambalo lina sehemu yake na kama haiwezekani kuzungumzia katika
sehemu yako ni vyema zaidi kukutana katika sehemu isiyo yenu wote.
Kuonekana nadhifu
Kuna
watu wanao amini kuwa tunapomsikiliza mtu akiongea huwa tunavutiwa
zaidi na kile anachosema kuliko anavyoonekana. Jambo hili siyo kweli.
Utafiti umeonyesha kuwa watu huvutiwa zaidi na muonekano wa msemaji
kuliko maneno anayosema. Hii ndiyo maana hata mavazi wanayovaa viongozi
wa dini huwasaidia kuongeza ushawishi wa maneno wanayosema kwa waumini
wao. Tunaposhawishi inafaa tuwe nadhifu.
Kujinasibisha na wale tunaowashawishi
Imebainika
kuwa unapokuwa ukijaribu kumshawishi mtu huna budi kumfanya akuone wewe
siyo tofauti na yeye na kwamba unamthamini yeye na mawazo yake. Ni
vyema ujenge hoja yako kuanzia kwenye fikra au mawazo yake.
Kuzingatia uelewa na uzoefu wa unayemshawishi
Watu
wenye uzoefu wa kushawishi huzingatia welewa na uzoefu wa mtu au watu
anaokusudia kuwashawishi. Huna budi kuelewa upeo wa welewa wa mtu
unayekusudia kumshawishi ili uweze kumshawishi vizuri zaidi. Huna budi
kuanzia hoja yako kwenye kiwango cha unayemshawishi na kumchukua
taratibu hadi kwenye mawazo yako.
Ni
vyema kukumbuka kuwa usipoweza kumweleza mtu au watu kwa kuzingatia
upeo wa welewa wake utakuwa umefanya kazi bure. Fikiri jinsi wazazi
wanavyopata shida ya kuwaeleza watoto wadogo mahali watoto wanakotoka.
Kila
mara wamezoea kusema watoto wananunuliwa sokoni au wanaokotwa porini.
Nakumbuka kuna mtoto mdogo alimuuliza mama yake mbona tumbo la shangazi
limekuwa kubwa, kwa sababu mama alijua shangazi akijifungua ataonekana
ana mtoto, akamjibu mtoto
“Katika
tumbo la shangazi yako kuna katoto kazuri” Yule mtoto akamuuliza mama
yake “Kama ni katoto kazuri kwa nini shangazi alikameza.” Hizi zote ni
jitihada za kuweza kupata maelezo yatakayolingana na uwezo wa kuelewa wa
mtoto
Tumia hoja za maarifa badala ya hoja ya fikira au mawazo yako
Unapotaka
kumshawishi mtu akubaliane na wazo lako huna budi kutumia maarifa ya
kweli badala kutoa hoja zinazoonekana kama hisia au mawazo yako tu.
Daima
hakikisha unatumia maelezo yenye ushahidi unakubalika. Maprofesa
hutumia ushahidi wa maarifa yaliyoandikwa katika vitabu na wataalamu
waliobobea katika fani mbalimbali. Viongozi wa dini nao hutumia maneno
yaliyoandikwa katika misahafu ya dini. Maneno yanayonukuliwa kutoka kwa
wabobezi na katika vitabu vitukufu hutumika kama hoja zenye nguvu
zinazosaidia kushawishi.
Tumia hadithi au mifano ya matukio halisi
Hakuna
kitu chenye nguvu ya kushawishi kama hadithi au mifano ya matukio ya
kweli. Vitu hivi huwa na nguvu ya kushawishi zaidi kuliko maelezo
yanayofafanua maarifa au dhana fulani. Hebu fikiria watu wawili
waliokuwa wakiuza magari yao walivyotofautiana katika kuyatangaza. Mmoja
alielezea ubora wa gari yake kwa kutumia maelezo ya yaliyowekwa na
watengenezaji kwenye kitabu cha gari.
Maelezo
hayo yalikuwa kama vile jinsi gari linavyotumia mafuta kidogo, jinsi
linavyokwenda kasi na kutulia barabarani bila kuyumba. Mwingine alieleza
ubora wa gari yake kwa kusema alijaza mafuta kwenye tanki akaenda hadi
Tanga na kurudi bila kuongeza mengine.
Alieleza
kwamba alitumia saa chache kwa sababu gari lake lilikuwa linakwenda
haraka kuliko magari mengine mengi. Pia kwa kuwa gari lake haliyumbi
hata kwenye kona nyingi aliweza kwenda kasi bila kuyumba hivyo alitumia
muda mfupi sana.
Huyu wa pili anaweza kuuza kwa urahisi kwa sababu anatoa mifano halisi ya jinsi gari inavyoweza kutumika.
Haya
niliyoyataja ni baadhi ya mambo ambayo mtu aliyatumia yatamsaidia
kuhamasisha watu wengine waafikiane na mawazo yake. Zamani watu
waliamini kuwa mtu hawezi kujifunza jinsi ya kushawishi watu kwa sababu
ni kipaji anachozaliwa nacho mtu. Lakini utafiti umedhihirisha kuwa
uwezo wa kushawishi unatokana na baadhi ya stadi za mawasiliano ambazo
mtu anaweza kujifunza mwenyewe kama nilivyoeleza katika makala hii.
MWANANCHI