Wa-Sudan Kusini waliokoseshwa makazi
Watu
waliokoseshwa makazi kutokana na mapigano katika mji wa Bor baada ya
kuwasili katika bandari ya Minkaman, nchini Sudan Kusin.
Katibu mkuu msaidizi wa masuala ya haki za binadamu, Ivan Simonovi amelitembelea taifa hilo lililogubikwa na mzozo wiki iliyopita. Amesema hali ni ya kusikitisha sana na kuelezea orodha ndefu ya manyanyaso ikiwemo mauaji, uchinjaji holela, ghasia za ngono, uchomaji, wizi wa ngawira na matumizi ya wanajeshi watoto.
Bwana Simonovic amesema ana matumaini kwamba katika muda wa wiki kadhaa watatoa ripoti ambayo itakuwa na baadhi ya matokeo ya awali kuhusu uchunguzi uliofanywa. Hadi sasa anasema kuna baadhi ya ushahidi na wana baadhi ya tuhuma ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kutosha.
Tayari anasema kwamba pande zote zimehusika na matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu.Simonovic amesema ripoti yake ya awali huenda isiweze kuwatambua wanaotuhumiwa kutenda maovu ambayo wakati mwingine itachukua muda zaidi.
Pia amesema kwamba Umoja wa Afrika-AU imependekeza kwa tume ya uchunguzi kuchunguza ukiukaji na kuzungumzia kiini cha mzozo.
Ghasia zilizuka katika taifa hilo changa katikati ya mwezi Disemba wakati Rais Salva Kiir alipomshutumu naibu wake wa zamani Riek Machar kwa jaribio la mapinduzi, dai ambalo Machar amelikanusha.
Tangu wakati huo mzozo umegeuka kuwa ghasia za kikabila ambazo zimehusisha makabila ya Nuer na Dinka na kusababisha vifo pamoja na raia kadhaa kukoseshwa makazi. http://www.voaswahili.com