Wizara ya Maliasili na Utalii, imetuma kikosi maalumu cha askari 20, ili kuongeza nguvu ya kuwasaka majangili walioua faru na kuchukua pembe zake, usiku wa kuamkia jana katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Imesema wiki iliyopita majangili watatu ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam, walikamatwa wakisafirisha kilo 37 za meno ya tembo katika gari ndogo, wakitoka mkoani Iringa kwenda katika jijini.
Pia imeeleza kuwa watu wanaodhaniwa kuwa ni majangili walioingia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro juzi alasiri ,wakiwa na bunduki aina ya SMG, walivamia basi la abiria na kuwapora wasafiri fedha na mali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema, “Baada ya kupokea taarifa hiyo usiku wa kuamkia leo (jana), wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, imechukua hatua ya kuanza msako mkali katika maeneo yote ya Serengeti na Ngorongoro na maeneo ya pembezoni,” alisema.
Nyalandu alisema magari na watu wanaoingia na kutoka katika hifadhi hizo lazima wapekuliwe kwa sababu wizara hiyo inawasaka raia watatu kutoka moja ya nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, baada ya kuonekana katika hifadhi hizo kwa nyakati tofauti.
“Tunawashuku raia hawa, lakini kwa sasa siwezi kusema wanatokea nchi gani. Hifadhi ya Serengati ina faru 32 pamoja na faru watano walioletwa na mradi maalum unaosimamiwa na Rais Jakaya Kikwete kutoka Afrika Kusini, ila faru mmoja kati ya hao watano aliuawa mwaka juzi,” alisema Nyalandu.
Alisema kuwa Serikali bado inarekebisha kasoro zilizojitokeza katika awamu ya kwanza ya Operesheni Tokomeza Ujangili na kjwamba awamu ya pili ya operesheni hiyo itaanza hivi karibuni baada ya kukamilika kwa maandalizi.