NYUMBA ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, inayotumiwa na mjane wake, Mama Maria na familia, wiki hii imevamiwa na vibaka usiku na kuvunjwa. Taarifa zilizofikia gazeti hili jana zilibainisha kuwa vibaka hao walipitia upande wa ufukweni usiku wa manane, wakavunja dirisha na kuingia.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, vibaka hao walitoweka na televisheni, ambayo
haikutajwa aina wala ukubwa na kompyuta ya mkononi aina ya Toshiba.
Akizungumza
na gazeti hili, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura, alisema nyumba hiyo ilivamiwa Januari 11 kati ya saa 8 usiku na
alfajiri.
Alithibitisha
kuwa wezi hao waliingia ndani ya uzio na kuiba televisheni na kompyuta
mpakato. Kamanda Wambura alisema kabla ya saa 8 usiku kuna watu walikuwa
macho, lakini baada ya muda walikwenda kulala na walipoamka asubuhi
wakakuta wameibiwa.
"Ndani
ya uzio huo kwa pembeni kuna nyumba anamoishi mjukuu wa Mwalimu
Nyerere, na huko ndiko waliingia na kuiba televisheni na hiyo kompyuta
baada ya kukata waya wa dirisha," alisema Kamanda Wambura.
Alisema taarifa ya tukio hilo imefunguliwa jalada katika kituo cha Polisi Oysterbay na kupewa namba OB/RB/822/2014.
Kamanda
alimtaja mjukuu wa Mwalimu aliyeibiwa kuwa ni Moringe Nyerere (30),
ambaye anafanyakazi katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF),
na anaishi katika nyumba hiyo.
Kwa
mujibu wa Kamanda Wambura, tayari mtu mmoja amekamatwa akihisiwa
kushiriki wizi huo ambaye hakumtaja jina, lakini alisema alipata kufanya
kazi katika nyumba hiyo na baadaye kufukuzwa.
"Kuna
kijana walimhisi kufanya wizi huo ambaye alikuwa akifanya kazi hapo kwa
karibu miaka miwili lakini alifukuzwa kutokana na tabia ya udokozi,
siku mbili kabla ya wizi huo alionekana hapo na alipoondoka wizi huo
ukafanyika," alisema Kamanda Wambura na kuongeza kuwa kuna mtuhumiwa
mwingine anatafutwa.
HABARI LEO