Dar es Salaam:
Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam, wanatajwa
kuwa wahusika wakuu wa kusaidia wahamiaji haramu kuingia nchini, kinyume
cha sheria.
Septemba
mwaka jana, mfanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali, Dominic Bomani
alimwambia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alipotembelea
uwanjani hapo kuwa wapo wahamiaji haramu ambao wamepewa nafasi nyeti za
ajira katika uwanja huo. Dk Mwakyembe aliahidi kufuatilia suala hilo.
Uchunguzi
wa Mwananchi umebaini kuwa polisi katika baadhi ya viwanja vya ndege
wamejenga mtandao na watumishi wengine, wakiwamo wa Idara ya Uhamiaji
ambao huwawezesha raia wa kigeni hasa kutoka nchi za Ethiopia, Somalia
na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kuingia nchini bila ya kuwa na
nyaraka zinazokubalika kisheria.
Tukio
la karibuni zaidi ni lile la kuingizwa nchini kwa raia watatu wa
Pakistani ambao licha ya kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa zamani
(Terminal – I) kutokana na kutokuwa na hati za kusafiria, wala nyaraka
zozote zinazowaruhusu kuingia nchini, baadaye waliachiwa na kuingia
nchini katika mazingira ya kutatanisha.
Chanzo
chetu uwanjani hapo kilisema: “Hawakuja na hati za kusafiria wala
nyaraka zozote na waliachiwa huru katika mazingira ya kutatanisha.”
Chanzo
hicho kiliwataja Wapakistani hao kuwa ni Hussein Amir, Ahmad Tahmir na
Shakeel Muhamadadi ambao walifika nchini, Oktoba Mosi, 2013 saa kumi na
moja jioni kwa ndege ndogo ya kukodi ambayo ilikuwa ikitokea Zanzibar.
Baada
ya kufika, walishukia Terminal 1 na baadaye kwenda kuswali katika
msikiti wa karibu, lakini kabla ya kutimiza azma yao hiyo, walikamatwa
na polisi kisha kufunguliwa hati ya kukamatwa (RB) namba JNIA/1005/2013.
Mapema
baada ya kuwasili kwao, wageni hao walipokewa na Dereva Teksi, Shami
Maringo ambaye alikiri kwamba aliagizwa kuwapokea, lakini kabla ya
kuanza safari waliomba kwenda msikitini kuswali kwa sababu ilikuwa
tayari ni saa 12:00 jioni.
Maringo
alisema aliwapokea raia hao watatu baada ya kupewa majina yao na
Mtanzania mwenye asili ya Asia ambaye alimwambia baada ya kuwapokea
awapeleke Kariakoo.
“Nilipewa
majina matatu kwenye karatasi na mhindi mmoja, nikaambiwa hao watu
watafika saa 10 jioni. Walipofika nikawatambua lakini tulikamatwa,”
alisema Maringo.
Maringo pia alikamatwa na kuambiwa kuwa ataachiwa baada ya mtu aliyemwagiza kuwapokea raia hao atakapofika.
Alisema
siku ya pili asubuhi, mtu huyo ambaye hata hivyo, alisema hamfahamu kwa
jina, alifika polisi na Maringo pamoja na raia hao waliachiwa huru.
Maringo anasema hakuweza tena kuwapeleka kwa sababu gari lake lilipata
pancha.
Uchunguzi
wa gazeti hili umebaini kuwa tukio la kukamatwa hadi kuachiwa kwa raia
hao wa Pakistani lilimhusisha Ofisa Upelelezi Kituo cha Polisi cha JNIA,
Denis Moyo.
Chanzo
chetu cha habari kinaeleza kuwa ili kufuta ushahidi wa tukio hilo,
taarifa za wahamiaji hao haramu hazikuandikwa katika kitabu cha rekodi
za polisi kama inavyotakiwa.
Kauli za wahusika
Kamanda
wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Seleman Hamis anasema taarifa hizo ni
za kushtua kwani hakudhani kama mambo kama hayo yanaweza kutendeka kwani
ulinzi mkali umewekwa uwanjani hapo.
“Nashukuru
kwa taarifa hizi, unajua nyinyi waandishi wa habari ni wa muhimu sana
katika habari za uchunguzi na mnaweza kutusaidia katika kazi zetu,”
alisema.
Kamanda
Hamis alisema inawezekana kabisa kuwa watu wanafanya vitendo vya
uhalifu huo pasipo polisi kufahamu. Hivyo wananchi hawana budi kutoa
ushirikiano ili kuutokomeza.
Moyo
ambaye pia ni Msaidizi wa Mkuu wa Makosa ya Jinai wa JNIA alipoulizwa
kuhusu madai hayo badala ya kujibu, aliuliza maswali mengi, huku akitaka
apewe majina ya baadhi ya wahamiaji hao.
Baada
ya kupewa, aliomba apewe dakika chache kisha apigiwe tena na
alipopigiwa simu baada ya dakika 20 alisema: “Nashukuru kwa taarifa
nitazifanyia kazi, ilimradi umenipa taarifa basi nitazifanyia kazi.”
Kabla
ya kutoa majibu hayo, ilisikika sauti ya mwanamke ambaye hakufahamika
ikimwelekeza: “Mwambie kwamba suala hilo litashughulikiwa.”
Mkuu
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa JNIA, Felisia Mtenga alikanusha
kuwapo kwa taarifa hizo na kusema hakuna suala kama hilo katika uwanja
huo ingawa alimtaka mwandishi kuzungumza na Moyo.
Kwa
upande wake, Meneja wa Usalama wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA), Clemence Jingu alisema hafahamu suala hilo na haliwezekani
kufanyika katika uwanja huo akisema ni lazima mgeni yeyote anayefika awe
na hati ya kusafiria, tiketi ya kurudi na viza.
Hata
hivyo, alisema hakuna tatizo iwapo wageni wanafika na ndege ya kukodi
wakitokea Zanzibar kwani uwanja wa huko unatakiwa kuhakikisha kuwa wana
nakala zote za kusafiria na wanapofika Dar es Salaam hufika kama watu wa
kawaida hivyo, hakuna haja ya kuangaliwa upya.
“Kila
uwanja wa kimataifa una sheria zake, akitua Zanzibar halafu akakodi
ndege kuingia Dar es Salaam, hana haja tena ya kuonyesha documents
(nyaraka) zake, anaingia kama mwenyeji tu,” anasema Jingu.
Alipoelezwa
kuwa wapo wahamiaji haramu wanaoingia kupitia JNIA moja kwa moja kutoka
nje alisema ni vigumu mno... “Haiwezekani wakawahonga, uhamiaji, polisi
wa uwanja wa ndege na kila mtu, ni vigumu. Lakini kama kuna suala kama
hilo sijalisikia na silifahamu. Zungumza na watu wa Uhamiaji.”
Msemaji
Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya
alipoulizwa alisema: “Tunashukuru kwa taarifa, lakini nafikiri tukipata
ushahidi kamili kama muda wa tukio, waliohusika na jinsi matukio hayo
yanavyofanyika, tutashukuru zaidi kwa sababu mtakuwa mmetusaidia.”
Mamlaka za Zanzibar
Kamishna
wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema ingawa ameishika nafasi hiyo
Zanzibar kwa muda mfupi lakini anafahamu kuwa kuna tatizo la wahamiaji
haramu.
“Ni
pana, linahitaji mshikamano wa kila kitengo. Kama wahamiaji wametokea
Pakistani lazima watakuwa wameanza kufanya mchezo huo tangu huko
walipotoka kwa hiyo ni tatizo mtambuka,” alisema Kamishna Makame.
Alisema
Uwanja wa Ndege Abeid Amani Karume unakabiliwa na uhaba wa watenda kazi
jambo ambalo alikwishapelekewa malalamiko na RPC wake.
Mkurugenzi
wa Uwanja huo, Juma Salehe alisema hajapata taarifa hizo... “Zipo
tuhuma za hapa na pale ambazo huwa tunazifanyia kazi na iwapo
zinatushinda tunazipeleka ngazi za juu, ingawa kwa tukio la hao raia wa
Pakistani, sijalisikia.”
Alisema
suala la wahamiaji haramu limesambaa kwani hata uhamiaji nao huenda
wanahusika kwani ndiyo wanaohakiki hati za kusafiria na visa.
MWANANCHI