TIMU ya Watafiti katika Chuo Kikuu cha North Carolina nchini Marekani,
wamegundua aina ya sumu ambayo ina uwezo wa kuua seli ambazo
zimekwishaathiriwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Sumu hiyo iliyopewa jina, 3B3-PE38, inaweza kutumika kutengeneza dawa
ambayo ikitumiwa na mtu aliyeathirika kwa VVU, itasaidia kuua virusi.
Watafiti wamebaini pia kuwa dawa hiyo itaweza kusaidia waathirika
kutolazimika kutumia dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARVs) maisha
yao yote.
Hii ni mara ya kwanza kwa wanasayansi kuweza kugundua sumu maalumu ya
kuua VVU. Tafiti nyingi zinazoendelea sehemu nyingi duniani ni za kupata
chanjo.
Kwa kawaida dawa ni sumu inayoua au kuathiri kiumbe kilichokusudiwa
wakati chanjo ni njia ya kuufanya mwili kutengeneza wenyewe kinga dhidi
ya vimelea, kulingana na aina ya ugonjwa.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa wiki hii na Taasisi ya Tafiti
za Kukabili Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID) ya Marekani, inasema
ni ugunduzi wa kipekee.
Upekee huo unaoelezwa unatokana na ukweli kuwa kwa sasa dawa zilizopo za
ARV zina uwezo wa kuzuia seli nyeupe iliyoshambuliwa isimamishe mvumo
wa kuzalisha virusi.
Walivyoendesha utafiti
Utafiti huo uliofadhiliwa na Taasisi ya Afya ya Taifa (NIH) ya Marekani,
unaelezwa kuwa panya 40 walitumika katika kutafiti 3B3-PE38.
Walichofanya watafiti hao ni kuwagawa panya kwenye makundi kadhaa na
kupewa dozi ya sumu ya 3B3-PE38 kwa viwango na muda tofauti kuanzia wiki
mbili hadi nne.
Baadhi walipewa ARV pekee na wengine walipewa pamoja na sumu hiyo ya 3B3-PE38.
Katika utafiti huo, walibaini kwamba wale ambao walitumia ARV pamoja na
sumu hiyo, waliweza kupunguza kwa kiwango kikubwa VVU pamoja na seli
ambazo tayari zimeathirika.Taarifa za awali zinaelezwa kuwa sumu hiyo
inaweza kusaidia kutibu watu walioathirika na mojawapo ya aina ya VVU.
Tuesday, January 21, 2014
CHUO KIKUU CHA NORTH CAROLINA CHAGUNDUA AINA YA SUMU YENYE UWEZO WA KUUA SELI ZILIZOATHIRIKA NA VURUSI VYA UKIMWI KWA BINADAMU BAADA YA KUFANYIKA KWA UTAFITI WA PANYA 40 NCHINI MAREKANI.
Unknown