Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Makundi
ya Urais wa 2015 yanaendelea kuivuruga CCM baada ya Mwenyekiti wa chama
hicho Mkoa wa Singida, Mgana Msindai kuibuka na kusema atamburuta
mahakamani Mwenyekiti mwenzake wa Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku
‘Msukuma’ asipomwomba radhi kwa kumchafua kwa kumwita mpuuzi.
Hata
hivyo, Kasheku amesema Msindai anaweza kwenda mahakamani huku
akisisitiza kwamba hawezi kumwomba radhi kwa kuwa anaamini kwamba
alichofanya ni kinyume cha taratibu za chama na vikao.
Juzi,
Kasheku alimponda Msindai mbele ya waandishi wa habari kwa kitendo
chake cha kusema kuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa yote ya Tanzania
wanamuunga mkono, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika safari
yake ya urais wa 2015 wakati wa sherehe ya mwaka mpya huko Monduli,
Arusha.
Msindai
alisema jana kuwa amemtaka Kasheku aitishe mkutano wa waandishi wa
habari na kumwomba radhi. “Asipofanya hivyo ndani ya siku saba
nitampeleka mahakamani,” alisema Msindai.
Msindai pia alikanusha kuwa aliwekwa kitimoto katika mkutano wa wenyeviti wa CCM wa mikoa uliofanyika Zanzibar.
Msindai
aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa miaka 15, alikiri kuwa
alialikwa pamoja na wenyeviti wenzake sita katika sherehe ya mwaka mpya
iliyoandaliwa na Lowassa huko Monduli.
Katika
sherehe hizo, Lowassa alitangaza kuwa ameanza safari ya matumaini,
kauli ambayo wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliitafsiri kama tangazo
la kuwania urais mwaka 2015.
Msindai
alikanusha kutangaza kuwa wenyeviti wote wa CCM wa mikoa wanamuunga
mkono Lowassa wakati wa sherehe hiyo... “Mimi ni Mwenyekiti wa wenyeviti
wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa wenyeviti wote wanamuunga mkono
Lowassa katika Uchaguzi Mkuu 2015... kikubwa tulichozungumza ni
kumuunga mkono katika safari yake ya mafanikio katika kuendeleza elimu,
maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai
alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na uwezo wake katika kusimamia
mipango yake ya maendeleo na zaidi katika kupigania elimu pana kwa
Watanzania.
“Alipokuwa
Wizara ya Maji alichangia maji kupatikana Dar es Salaam na mikoani na
maendeleo mengi, uwajibikaji kwenye jimbo lake na aendelee hivyo...hayo
ndiyo tuliyomsifia. Nilizungumza haya na sitabadilika,” alisema Msindai,
ambaye alisema haogopi kufukuzwa.
“Mimi
si mpya ndani ya CCM kama ‘Msukuma’. Nina miaka zaidi ya 40, ninaelewa
taratibu zote za chama za udiwani, ubunge na urais. Kama ni kampeni ni
baada ya chama kumpitisha mtu na sisi tutamuunga mkono... hata mimi
ninaweza kuwania urais,” alisema.
Siombi radhi
Kwa
upande wake Kasheku alisema hamwombi radhi Msindai, kwani si wenyeviti
wote wa CCM wanaomuunga mkono Lowassa katika safari yake aliyoiita ya
matumaini.
“Siombi
radhi na hata sasa hivi anaweza kushtaki, tulipokutana Zanzibar
alitueleza kuwa alitoa kauli ya kuumuunga mkono Lowassa kimakosa na
kusema alikuwa akimaanisha yeye na wenzake aliokwenda nao Monduli ndiyo
wanamuunga mkono Lowassa,” alisema Kasheku.
Kasheku
alifafanunua kuwa Msindani alisema kuwa wanahabari walikosea kumnukuu
baada ya kuandika katika vyombo vya habari kuwa alisema wenyeviti wote
wanamuunga mkono Lowassa.
Alisema
baada ya Msindai kukiri jambo hilo, wenyeviti waliokuwa Zanzibar
waliandaa tamko la pamoja na kuagiza lisomwe na Msindai mbele ya
wanahabri katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Dar es Salaam.
“Katika
huo mkutano ilitakiwa niwepo mimi (Kasheku), Msindai na Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, ila cha ajabu mwenzetu
(Msindai) alitukimbia na tulipomtafuta akasema yupo Singida, hivyo sisi
tuliamua kutoa tamko lile,” alisema Kasheku.
Alisema
kauli aliyoitoa Msindai ni kinyume na maagizo ya wenyeviti wote wa CCM,
huku akimtaka kabla ya kwenda mahakamani, ahakikishe kuwa amewasilisha
malalamiko yake ndani ya chama ili Kamati ya Maadili ya chama ikae na
kutoa uamuzi.
“Hatuna
ugomvi na Lowassa, tuna ugomvi na yeye aliyetuweka nyuma yake na kusema
wote tunamuunga mkono Lowassa, nani alimwambia maneno hayo na ilikuwa
katika kikao gani?,” alihoji Kasheku na kuongeza:
“Kama
kuna watu wapo nyuma ya Lowassa au mtu yeyote ni siri yao, iweje yeye
atulazimishe sisi kuwa nyuma yake kwa mgongo wa Mbunge wa Monduli”.
Mgeja amtetea Msindai
Mwenyekiti
wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja ambaye pia alikuwa Monduli,
alimtetea Msindai akisema hakuwahi kuzungumzia suala la urais katika
mkutano huo wa Monduli zaidi ya kumsifu Lowassa kwa mafanikio aliyoleta
kwenye jimbo lake na maeneo mengine alipokuwa Waziri Mkuu.
Alisema
hakuna dhambi kwa kumpenda mtu yeyote, wote wanaotoa kauli za kukanusha
ni dalili za woga, wivu, kutokujiamini na inawezekana wana watu nyuma
yao.
MWANANCHI