Katibu
Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa na mwenyekiti wake Freeman Mbowe
wakielekea kuzungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama
hicho Dar es Salaam jana kuhusu kuanza kwa ‘Operesheni Pamoja Daima’ ya
kuzunguka nchi nzima ili kuimarisha chama hicho. Picha na Fidelis
Felix
Dar es Salaam. Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo, kinarusha helkopta
tatu kwa siku 14 mfululizo, katika kutekeleza kampeni iliyopewa jina la
Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini.
Ziara
hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku viongozi wa
chama hicho wakijigawa katika makundi sita; matatu yakitumia helkopta
na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia usafiri wa magari.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, lengo
la operesheni hiyo ni kukiimarisha chama hicho na kuwafumbua macho
wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Viongozi
wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda
kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake katika operesheni hii. Tutafanya
mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza kuongeza wiki nyingine moja.”
Alisema
chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi wengi kadri
itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wake wa
ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata
27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
“Naomba
tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni hata kidogo, huu ni mwendelezo
wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa
na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa
2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa
sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi. Makundi
yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, tutapita kila Kata
ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe
alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika Jimbo la Kalenga ambalo
kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye pia alikuwa Waziri wa
Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu
nchini Afrika Kusini.
“Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza kufanyika uchaguzi katika jimbo
hilo, Chadema tutafika Kalenga na tutafanya mkutano maalumu na kutoa
pole kwa wakazi wa jimbo hilo kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,”
alisema Mbowe.
Operesheni
hiyo inafanyika siku chache tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini
kipite katika mgogoro ambao ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wake, Zitto Kabwe kukimbilia mahakamani ili kunusuru uanachama wake.
Wakati
Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na zuio la mahakama, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati
Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa uanachama, likiwa ni hitimisho la
mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa zao pamoja na Zitto.
Daftari la wapigakura
Mbowe
alisema msimamo wa chama chake ni kutaka daftari la kudumu la
wapigakura lifanyiwe marekebisho kabla ya kupigwa kwa kura za maoni kwa
ajili ya kupitisha Katiba Mpya.
“Tutagomea
upigaji wa kura na tutawahamasisha wananchi kugomea kupiga kura.
Serikali ya CCM isijidanganye kwa kuweka mikakati ya kukwamisha zoezi
hili,” alisema Mbowe.
Alisema
kama Serikali inataka amani iendelee kuwepo isifanye mzaha katika
mchakato wa Katiba Mpya kwa maelezo kuwa Katiba siyo mali ya vyama vya
siasa, bali ni mali ya wananchi.
“Katiba
siyo ya Chadema, CUF wala NCCR-Mageuzi. Sheria inaeleza wazi kwamba
daftari la wapigakura ni lazima lifanyiwe marekebisho mara mbili baada
ya Uchaguzi Mkuu na kabla ya kuanza Uchaguzi Mkuu mwingine lakini hilo
halijafanyika mpaka sasa licha ya Uchaguzi Mkuu kufanyika miaka minne
iliyopita,” alisema Mbowe.
Alisema
wapo Watanzania waliohama maeneo yao ya awali, waliopoteza
vitambulisho, waliofikisha umri wa kupiga kura na kusisitiza kuwa
kuwaacha watu hao nje ya mfumo wa kupiga kura ni kuwanyima haki yao ya
Kikatiba.
“Kwa
mujibu wa utafiti tulioufanya tumebaini kuwa wapo watu zaidi ya milioni
5 wanaohitaji kuingizwa katika daftari la wapigakura,” alisema Mbowe na
kuongeza;
“Kama Katiba haitapita kwa sababu ya kutokuboreshwa kwa daftari la wapigakura hatutarudi katika Katiba ya sasa hiyo ni ndoto.”
MWANANCHI